
Watu wengi hufikiri kuwa Ngono ya Mdomo ni salama zaidi kuliko aina nyingine za ngono, lakini ukweli ni kwamba inaweza kuwa chanzo cha maambukizi hatari. Moja ya maambukizi hayo ni virusi vya HPV (Human Papillomavirus), ambavyo huambukizwa kwa njia ya mgusano wa ngozi na ngono, ikiwemo ngono ya mdomo.
Virusi hivi vipo vya aina zaidi ya 200, na baadhi yake huhusishwa na maambukizi kwa binadamu yanayoweza kupelekea saratani za aina mbalimbali ikiwemo Saratani ya Koo, Mlango wa Kizazi na Koo.
HPV huweza kusababisha masundusundo ya kinywa, ambayo ni uvimbe mdogo au wa makundi unaoota kwenye midomo, ulimi au ndani ya mashavu. Hali hii siyo tu kwamba huonekana vibaya, bali pia inaweza kusababisha maumivu na usumbufu. Zaidi ya hapo, baadhi ya aina za HPV, hasa aina ya HPV-16 imehusishwa moja kwa moja na Saratani ya Koo.
Saratani hii huathiri maeneo kama tonsils, sehemu ya nyuma ya ulimi na koo la kati. Maambukizi haya yanaweza kuchukua miaka kuonyesha dalili, na mara nyingi hukutwa baada ya saratani kuwa imekua.
Kwakuwa utamaduni wa kushiriki tendo la ndoa kwa njia ya mdomo unazidi kushika kasi, hasa miongoni mwa vijana, ni muhimu kukumbuka kuwa njia hiyo si salama ukiachia maambukizi ya HPV ambayo tumeyajadili hapa, inaweza pia kusababisha uambukizanaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU).
Kila unapofikiria kufanya ubunifu mpya kunogesha mapenzi yako kwa mtu unayempenda, fikiria kuhusu afya yako kwanza, na ikiwezekana chukua tahadhari zote kujilinda kwani afya yako ndiyo utajiri wako wa kwanza.
