Usiruhusu Wageni Wabusu Mtoto Mchanga, ni Hatari

Busu linaweza kuonekana kama ishara ya upendo, lakini kwa mtoto mchanga linaweza kuwa hatari.

Mfumo wa kinga mwili wa Watoto wachanga huwa bado haujakomaa vizuri hivyo wanaweza kuambukizwa kwa urahisi vimelea kama Virusi, mafua, au bakteria wengine kutoka kwa watu wazima.

Mathalani, ndani ya miezi 3 ya mwanzo, seli nyeupe za kupambana na maambukizi hasa neutrophils na monocytes huwa chache sana kuliko watu wazima. Hii inatoa maana kuwa, ugonjwa unaoweza kuonekana wa kawaida kwa mtu mzima unaweza kuwa wa hatari kubwa kwa mtoto mchanga, pengine hata kuhatarisha maisha yake.

Virusi vya herpes ni mfano hai, ambavyo Pamoja na sehemu zingine huathiri vikali njia ya hewa, na ikitokea mtoto amevipata vinaweza kuathiri macho, midomo na Ngozi yake kwa kiwango kikubwa.

Lakini pia fikiria tu, hauwezi kujua mtu anaye busu mtoto wako katoka wapi. Vipi kama ametoka kushiriki tendo la ndoa na mweza wake, vipi kama ametoka kubusiana na mtu mwingine ambaye pia hali yake ya kiafya haijulikani?

Kuwaelewesha wageni wanaokutembelea kuwa hairuhusiwi kubusu mwanao si ishara ya majivuno, ni sifa njema ya wazazi wanaojua staha na kujali afya ya mtoto wao.

Njia salama ni kuwaomba wageni wamwangalie tu mtoto, wamsalimie kwa mbali, au wamguse kwa mikono safi, bila kumbusu. Hatua hii ndogo inaweza kusaidia kumlinda mtoto dhidi ya maambukizi hatarishi katika wiki na miezi ya mwanzo ya maisha.