Veriafya ni shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalofanya kazi Tanzania, lililoanzishwa kwa lengo la kuimarisha mawasiliano ya afya na uadilifu wa taarifa za afya. Jina Veriafya limetokana na maneno Verify (thibitisha) na Afya (health), likiwa na maana ya kuthibitisha na kusambaza taarifa sahihi za afya kwa jamii.
Tunatambua kuwa kuenea kwa taarifa potofu zisizo na Ushahidi wa kisayansi kuhusu afya ni tishio kubwa kwa ustawi wa watu, kwani husababisha mkanganyiko na kuhatarisha maisha. Kupitia Veriafya, tumejikita katika kutoa taarifa za afya zilizo sahihi, zenye ushahidi wa kisayansi, zilizo rahisi kueleweka, na zinazozingatia muktadha wa kijamii na kiutamaduni wa Watanzania.
Dira yetu ni kuona jamii yenye afya bora inayowezeshwa na taarifa za afya zilizo sahihi na zinazoaminika. Dhamira yetu ni kuwapa wananchi taarifa za afya zilizothibitishwa, zinazolingana na mazingira yao, ili waweze kufanya uamuzi sahihi kuhusu afya na ustawi wao.
Veriafya inafanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuzuia magonjwa, kuhamasisha mitindo bora ya maisha, kukuza Afya ya Uzazi na Haki za Uzazi (SRHR), kuboresha uelewa wa afya kidijitali, kujenga uwezo wa wanahabari na wahudumu wa afya katika uthibitishaji wa taarifa, pamoja na kusaidia jamii kukabiliana na dharura za afya kwa kutoa taarifa za haraka na sahihi.
Kupitia ushirikiano na serikali, vyombo vya habari, taasisi za afya, mashirika ya kiraia, na jamii kwa ujumla, Veriafya inalenga kujenga jamii iliyoelimika, yenye imani na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi ya afya kwa maendeleo ya taifa lenye afya na uimara.
