
Mada hii inaweza isieleweke kirahisi kwa baadhi ya watu kwakuwa hawajawahi kuona, pia kutokana na uwepo wa imani za kitamaduni zinazokinzana na sayansi ya tiba.
Hata hivyo, ni ukweli ulio wazi kuwa baadhi ya Wanaume huweza kuonesha dalili zinazofanana na za Ujauzito wakati wake zao wakiwa na Mimba. Hali hii inajulikana huitwa mimba ya huruma, au kitaalamu kama Couvade Syndrome na huambatana na dalili nyingi za Ujaizito ikiwemo Kichefuchefu, Kutapika, Maumivu ya tumbo, Uchovu, Kuvimbiwa na Mabadiliko ya Hisia. Ingawa si Ujauzito halisi, dalili hizi hujidhihirisha mwilini kama mwitikio wa kihisia unaoendana na ujauzito wa mwenza.
Mabadiliko haya huweza kuchochewa na ukaribu wa kihisia kati ya wenza, hasa pale Mwanaume anaposhiriki kikamilifu katika safari ya Ujauzito kama kuhudhuria Kliniki, kushiriki maandalizi ya Mtoto au kuonesha hisia kubwa juu ya ujio wa Mtoto.
Hali hii si Ugonjwa wala hatari kiafya, na mara nyingi dalili huanza kupungua kadri Ujauzito unavyokaribia mwisho au pindi mtoto anapozaliwa. Hata hivyo, ikiwa dalili zinakuwa nzito au zinasababisha usumbufu mkubwa, ni vyema kupata ushauri wa kitaalamu.
