Tangu miaka ya 2000 Kabla ya Kristu, nchi ya India ilikuwa inatumia mti wa mlonge kwenye kutibu magonjwa mbalimbali yanayo mkabili binadamu.
Kwa mujibu wa tafiti, majani ya mlonge huwa na vitamini A mara nne zaidi kuliko iliyopo kwenye karoti, mara saba zaidi ya vitamini C kuliko iliyopo kwenye chungwa, mara 4 zaidi ya madini ya calcium kuliko yale yaliyopo kwenye maziwa na protini inayopatikana humo ni nyingi mara mbili zaidi kuliko ile ya yogurt.
Baadhi ya sehemu huuita mti huu kama “mti wa maajabu”.
Kwa sasa mti huu umesambaa sehemu nyingi duniani.
Afrika, Asia na Marekani ya Kusini ni miongoni mwa mabara yenye kiasi kikubwa cha mlonge.
Virutubisho
Ni mti ulio na madini chuma, vitamini A, zinc, magnesium, potassium, calcium, asidi ya foliki, vitamini C, B6 na protini.
Huwa pia na kemikali za oleic acid, gallic acid, tocopherols, ethyl acetate (EtOAc), rutin, luteolin, quercetin, apigenin pamoja na kaempferol.
Zifuatazo ni faida za Mlonge kwa afya;
1. Sumu
Huulinda mwili kwa kuondoa sumu zinazoshambulia seli, pamoja na kusababisha magonjwa sugu.
Ifahamike kuwa seli ndio kitovu cha uhai wa binadamu. Zinapo shambuliwa huhatarisha uhai, na kufanya afya ya binadamu iwe dhaifu.
Mlonge huharibu kemikali na sumu hatarishi hivyo kuzilinda seli za mwili.
2. Uvimbe
Sehemu zote za mlonge zinaweza kuuamsha mwili katika kupambana na mwamsho unaoweza kuchochea uvimbe.
Kemikali za isothiocyanates hutajwa kuhusika moja kwa moja katika kukamilisha kazi hii.
Hufanya hivyo kwa kudhibiti NO, PGE2, cytokines pia huzuia kuvunjwa kwa IκB-α kwenye mfumo wa taarifa za NF-κB. (1,2,3)
Mambo hayo ndio huchochea kutokea kwa uvimbe.
3. Sukari
Kisukari ni ugonjwa hatari kwa afya.
Usipodhibitiwa vizuri unaweza kuleta athari za kudumu kwa afya pamoja na kifo.
Tafiti nyingi zilizofanyika kwa wanyama zinabaibisha uwezo wa mlonge katika kudhibiti ongezeko la sukari, pamoja na kuleta ahueni kwa wagonjwa. (4)
Hata hivyo, tafiti nyingi zaidi kwa binadamu zinahitajika kufanyika ili kuoanisha taarifa hizi.
4. Ini
Ini la binadamu hufanya kazi zaidi ya 500 mwilini.
Huzalisha nyongo, hutoa sumu mwilini, huchuja damu inayotoka kwenye mfumo wa chakula pamoja na kudhibiti mifumo mingi ya mwili.
Ni muhimu ini likilindwa.
Mlonge hulinda ini pamoja na kuimarisha afya yake dhidi ya mashambulizi ya vimelea vya magonjwa, pombe na madawa.
5. Saratani
Sifa kuu ya mlonge katika kudhibiti saratani hutokana na uwepo wa kampaundi za niazimicin.
Huwa na ufanisi mkubwa katika kupambana na aina mbalimbali za saratani hasa zile za matiti na utumbo mkubwa. (5)
Epuka ugonjwa huu sugu kwa kutumia mlonge.
6. Mafuta
Huharibu mafuta mabaya mwilini.
Katika utafiti mmoja, matumizi ya mbegu za mlonge yaliongeza utolewaji wa mafuta mabaya mwilini kupitia choo.
Majani yake yanaweza kutumika pia kwa kazi hii.
Hufaa sana kwa watu wenye changamoto ya kuwa na mafuta mengi yasiyofaa mwilini. (6,7)
Kwa kuwa mfumo wa damu kwa ujumla huhusisha pia moyo kwa kiasi kikubwa, mlonge utaulinda moyo wako.
7. Vimelea
Mlonge huwa na uwezo wa kupambana na vimelea vya magonjwa hasa bakteria na fangasi.
Kwa upekee kabisa, bakteria jamii ya Enterococcus faecalis ambao husababisha maambukizi kwenye mfumo wa mkojo, uti wa mgongo, kuta za moyo pamoja na mchafuko wa damu hudhibitiwa kikamilifu na mlonge. (8)
Hupambana pia na bakteria wanao sababisha vidonda vya tumbo
8. Presha
Kampaundi za niaziminin na isothiocyanate hulinda mishipa ya damu na kuiimarisha.
Aidha, huzuia kujaa kwa mafuta yasiyo faa pamoja na kushusha shinikizo la kubwa la damu. (9,10)
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu bilioni 1.28 dunuani wanaishi na changamoto ya shinikizo kubwa la damu. Chukua tahadhari.
9. Damu
Mlonge husaidia kuongeza damu mwilini.
Ni mti wenye kiasi kikubwa cha madini ya chuma ambayo mwili wa binadamu hutumia kuzalisha damu.
10. Kinga
Mwili huwa na askari wake wanaosaidia kwenye kuulinda kila siku, mchana na usiku.
Askari hawa hupaswa kuwa tayari muda wote kukabiliana na mashambulizi ya vimelea vya magonjwa.
Kwa kuwa hufanya kazi hii pasipo kupumzika, ni lazima nguvu ya ziada itumike kwenye kuwapatia msaada wa nguvu za ziada.
Unakumbuka tulisema nini kwenye utangulizi?
Mlonge huwa na zinc pamoja na kiasi cha vitamini C mara saba zaidi kuliko ile ya chungwa. Hutumiwa na mifumo ya mwili katika kuimarisha kinga yake kwenye kupambana na magonjwa. (11)
Ongeza kinga ya mwili wako kwa kutumia mmea huu.
11. Vitamini A
Vitamini A hutoa mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya binadamu.
Huhitajika kwenye kuboresha afya ya macho, kutunza ngozi, afya ya uzazi, mfumo wa kinga mwili pamoja na kuboresha utendaji kazi wa viungo vya mwili hasa figo, moyo, kibofu, sikio la ndani na mapafu.
Kwa kuwa huwa na kiasi kikubwa cha viondoa sumu, huusaidia mwili katika kuzuia na kupambana na magonjwa sugu mfano kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani. (12,13)
Huusaidia mwili kwenye kutengeneza askari wake wa kupambana na magonjwa wanaofahamika zaidi kama T helper cells, aina ya seli nyeupe za damu.
Hufanya pia kazi ya kuwasambaza askari hawa sehemu mbalimbali za mwili.
12. Mifupa
Asilimia 99 ya mifupa na meno hufanywa kwa madini ya calcium.
Huongeza ubora wa afya ya mifupa, kuunganisha mifupa, kuongeza ujazo wake pamoja na kupunguza changamoto za kuvunjika kirahisi. (14)
Huongeza ubora wa meno. Watu wenye kiasi kidogo cha calcium hukumbwa na matatizo ya kupoteza meno yao kuliko wale wenye kiasi cha kutosha cha calcium.
Mlonge unafaa kwa afya bora ya meno na mifupa yako.
Tahadhari
Taarifa za usalama wa mlonge kwa wanawake wajawazito pamoja na wale wanao nyonyesha huwa hazipo wazi sana.
Hivyo kwa sababu za kiusalama, makundi haya yanashauriwa kuepuka matumizi makubwa ya mmea huu ili kujiweka salama.

