Hispania ni nchi ya kwanza duniani inayoongoza kwa uzalishaji wa mafuta ya mzeituni.
Mafuta haya huvunwa kutoka kwenye miti ya mizeituni ambayo historia inaitaja kuanza kulimwa zaidi ya miaka 3500 kabla ya Kristu.
Virutubisho
Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), pamoja na tafiti mbalimbali, mafuta ya mzeituni huwa na sodium, vitamini K na E, omega 6, Omega 3, oleic acids, linoleic acids pamoja na madini chuma.
Zaituni huwa na faida nyingi kwa afya, baadhi yake ni hizi;
1. Moyo
Mafuta ya mzeituni huwekwa kwenye kundi kubwa ambalo kwa lugha za kitaalam huitwa Mediterranean diet, yaani mlo wa kimeditereniani.
Huitwa mlo wa kimeditereniani kwa kuwa wanaopakana karibu na bahari ya meditereniani. Huhusisha vyakula vya asili vya baharini hasa samaki, matunda na mboga za majani.
Mafuta ya mzeituni kama sehemu ya mlo huu huulinda moyo, huharibu lehemu mbaya, huimarisha mishipa ya damu, pamoja na kuzuia kuganda kwa damu. (1,2,3)
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa watu milioni 19.7 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa ya moyo.
Takwimu hizi zinatisha, chukua tahadhari.
2. Presha na Kiharusi
Kiharusi kinaweza kusababishwa na kuganda kwa damu hivyo kuzuia usafirishwaji wake kwenye ubongo, au kuvujia kwa damu kwenye ubongo.
Kutokana na tabia yake ya kuimarisha mishipa ya damu pamoja na kuimarisha afya ya moyo, mafuta haya husaidia kupunguza shinikizo la juu la damu ambalo lisipo dhibitiwa vizuri husababisha kutokea kwa kiharusi. (4,5)
Kama unatoka kwenye ukoo, familia au kama hali yako ya afya inaonesha dalili ya kutokea kwa presha, anza sasa kutumia mafuta ya mzeituni.
3. Sumu
Mojawapo ya vitamini muhimu zinazopatikana kwenye mafuta ya mzeituni ni vitamini E ambayo kitaalamu hutumika kama kiondoa sumu cha mwili.
Viondoa sumu hivi huulinda mwili dhidi ya magonjwa sugu, hulinda seli za mwili pamoja na kulinda vinasaba vya mwili ambavyo hutunza taarifa muhimu za urithi wa kila kiumbe hai duniani.
4. Uvimbe
Kemikali za oleocanthal zinazopatikana kwenye mafuta ya mzeituni hufanya kazi kama zilivyo dawa za kuondoa uvimbe na maumivu kama ibuprofen.
Kemikali za oleic acid hufanya kazi ya kudhibiti viunganishi vya mwili vinavyochochea uvimbe. (6)
Ni mafuta muhimu sana unayopaswa kuyaongeza kwenye mlo wako wa kila siku.
5. Uzito
Mafuta mengi tunayotumia majumbani kwetu huchangia ongezeko la uzito wa mwili unaoweza kusababisha uzito uliozidi, kitambi na kiribatumbo.
Mafuta ya mzeituni hayapo hivyo. Ni aina ya mafuta inayotajwa na tafiti nyingi kuwa na sifa kubwa ya kutokusababisha ongezeko la uzito. (7,8)
Husaidia kutunza uzito sahihi wa mwili.
6. Kisukari
Mafuta ya mzeituni huulinda mwili usipatwe na tatizo la kisukari.
Pia, huongeza uwezo wa vimeng’enya vya insulini ambavyo hutumiwa na mwili katika kudhibiti ongezeko la sukari.
Kisukari ni ugonjwa unaotesa watu wengi duniani, epuka kuwa mmoja wao.
7. Saratani
Nchi nyingi zinazopatikana karibu na bahari ya meditereniani huwa na sifa kubwa ya kuwa na namba ndogo ya waathirika wa aina fulani za saratani.
Sifa hii huhusishwa na matumizi makubwa ya mafuta ya mzeituni.
Hata hivyo, tafiti nyingi za kisayansi zinahitajika kufafanua zaidi madai haya.
8. Bakteria
Mafuta ya mzeituni huwa na kemikali zenye uwezo wa kudhibiti ukuaji wa aina mbalimbali za bakteria.
Mojawapo ya bakteria hao ni H. pylori ambao husababisha vidonda vya tumbo.
Majibu ya tafiti mbalimbali yanaonesha kuwa aina hii ya mafuta huwa na uwezo wa kupambana na walau aina nane za bakteria, huku aina tatu kati yake zikiwa na usugu wa kutibiwa kwa dawa za kawaida. (8)
Muhtasari
Mafuta haya ni bora sana kwa afya.
Wengi wamezoea kuyatumia kwa massage na urembo pasipo kujua kuwa hutumika pia katika kuandaa vyakula.
Anza sasa kuyatumia.

