Mtoto Kupiga Kwikwi ni Jambo la Kawaida, ni Hatua za Ukuaji

Mtoto kupiga kwikwi ni jambo la kawaida na mara nyingi si hatari, hutokea kwa sababu misuli ya kupumua (Diaphragm) ya mtoto huwa bado haijakomaa vizuri, hasa katika miezi ya mwanzo ya maisha.

Mara nyingi kwikwi husababishwa na mtoto kunyonya haraka, kushiba kupita kiasi, kumeza hewa wakati wa kunyonya, au mabadiliko ya ghafla ya joto. Hali hii kwa kawaida haimsababishii maumivu wala usumbufu mkubwa.

Kwa kawaida, kwikwi huisha yenyewe bila dawa wala matibabu maalum. Mzazi anaweza kumsaidia mtoto kwa kumnyonyesha polepole, kuhakikisha anacheua baada ya kunyonya, kama kafikia umri wa miezi 6 na kuendelea unaweza kumpa maji pamoja na kumweka katika mkao wa wima kwa dakika chache.

Dalili hatarishi

  • Kwikwi zinazoendelea kwa zaidi ya saa 48.
  • Kwikwi zinazosumbua kula, kulala au kupumua.
  • Kuambatana na dalili mpya kama maumivu ya kifua, maumivu makali ya tumbo, kutapika, kupumua kwa shida (dyspnoea), kuharisha, au kupungua uzito bila sababu.

Hali hizi zinaweza kuashiria matatizo makubwa ya kiafya kama changamoto kwenye mishipa ya fahamu, magonjwa ya mfumo wa neva (ubongo au uti wa mgongo), au matatizo mengine makubwa zaidi mwilini.

Pia, baadhi ya Watoto huanza kuonesha dalili za kupooza upande fulani wa mwili, kushindwa kuongea na kucheza Pamoja na kudhoofika sana kwa mwili. Katika hali hizi, mfikishe hospitalini haraka kwa uchunguzi na matibabu.