Juisi ya Miwa Huchacha Mapema, Chanzo cha Maumivu ya Tumbo

Miongoni mwa vinywaji vinavyovutia kutumia hasa nyakati za Joto kali ili kupoza mwili ni Juisi ya Miwa. Sifa kubwa ya juisi hii si utamu pekee, bali ni uwezo wake wa kuupa mwili nishati kubwa kutokana na uwepo wa sukari za asili za Sucrose, ambazo mwili huzivunja kuwa Glucose na Fructose.

Ubora wa juisi ya Miwa umepambwa kwa virutubisho vingine ikiwemo viondoa sumu, nyuzilishe, vitamini na madini muhimu kama zinki na madini chuma, ambavyo vyote ni muhimu kwa afya ya mwili. Kama haujawahi kutumia juisi hii, unaweza kuanza kuizingatia sasa ili unufaike na ubora wake.

Hata hivyo, Juisi hii huchacha haraka ikiwa itaachwa muda mrefu bila kuhifadhiwa vizuri baada ya kutengenezwa, hivyo kusababisha madhara kwa afya ikiwemo Maumivu makali ya tumbo, kuhara, kichefuchefu, kiungulia na kutapika pamoja na maumivu ya kichwa na kizunguzungu.

Miongoni mwa viashiria vya Juisi iliyochacha ni uwepo wa Harufu kali au inayofanana na pombe, ladha kali na mbaya isiyo ya kawaida, Povu kuongezeka pamoja na Mabadiliko ya rangi.

Kuzuia hali hii, unashauriwa kunywa mara tu baada ya kukamua, ndani ya dakika 20–30, Kuiweka kwenye friji ikiwa hutaitumia mara moja pamoja na Kutumia vyombo visafi sana inapokamuliwa. Ukiona imeanza kuwa na harufu au ladha ya ajabu, usinywe, tayari imeanza kuchacha.

Tahadhari

Utafiti uliofanywa mwaka 2021 na Chuo Kikuu Katoliki cha Sayansi za Afya na Tiba Bugando (CUHAS) ulibaini baadhi ya waandaaji wa juisi hii kwenye Wilaya ya Nyamagana walikuwa hawazingatii usafi, na juisi hii ilibainika kuwa na masalia ya vinyesi.

Utafiti huu unatoa picha pana kuhusu maandalizi ya juisi hii hivyo ni muhimu kuwa makini hasa unaponunua kwenye mazingira yasiyo masafi.