Kwa Mtoto Chini ya Miaka 5, Yai la Kuchemsha ni Bora kuliko la Kukaanga

Kwa afya bora ya Mtoto, hasa mwenye umri wa chini ya Miaka 5, yai lililochemshwa ndilo chaguo linalofaa zaidi kuliko yai la kukaanga.

Yai la kuchemsha hupikwa bila mafuta, Jambo linalolifanya kuwa salama na lishe safi kwa mtoto, tofauti na yai la kukaanga ambalo mara nyingi hutumia mafuta mengi ambayo si rafiki kwa afya ya mtoto mdogo.

Aidha, huwa rahisi kumeng’enywa na tumbo la mtoto, na husaidia kupunguza uwezekano wa matatizo ya tumbo au mzio. Mbali na hilo huhakikisha halina vimelea hatari kama Salmonella, hivyo kumkinga mtoto dhidi ya maradhi yanayoweza kusababishwa na mayai ambayo hayajapikwa kikamilifu.

Ifahamike kuwa, bakteria jamii ya Salmonella ni maarufu sana kwa kusababisha sumu ya chakula na maumivu makali ya tumbo yanayoweza pia kupelekea kuharisha, kupoteza maji na chumvi muhimu za mwili na kwa baadhi hasa isipotibiwa mapema inaweza kupelekea kifo.

Kwa upande mwingine, yai la kukaanga linaweza kuwa na ladha nzuri lakini si chaguo bora kwa mtoto mdogo, hasa linapotengenezwa kwa mafuta mengi au linaongezewa viungo vikali na chumvi, ambavyo vinaweza kudhuru afya ya Mtoto. Mafuta yaliyounguzwa huwa na hatari ya kusababisha magonjwa ya moyo na chumvi ikichangia kwa kiasi kikubwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza hasa Presha.

Kwa ujumla, wazazi au walezi wanashauriwa kumpatia mtoto yai lililochemshwa vizuri kama sehemu ya mlo wake wa kila siku ili apate protini ya kutosha kwa ukuaji wa mwili na ubongo.

Ingawa yai la kukaanga linaweza pia kuliwa na watoto, inashauriwa lisiwe limetengenezwa kwa kuwekewa mafuta mengi, viungo na chumvi.