Hospitali ya Temeke Kuchunguzwa kwa Rushwa na Udhalilishaji wa Wagonjwa

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ameagiza kufanyika kwa Uchunguzi Hospitali ya Temeke kufuatia tuhuma mbalimbali zinazoikabili.

Siku za hivi karibuni, kumebainika utendaji usioridhisha katika Hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuzimwa kwa mashine ya X-Ray, ambapo pia ufuatiliaji wa siri wa Waziri Mchengerwa umebaini uwepo wa rushwa za wazi wazi bila uoga kuanzia kwa baadhi ya walinzi wasio waaminifu mpaka kwa baadhi ya watoa huduma na kauli mbaya zinazotolewa na walinzi hao na watoa huduma kwa wagonjwa. Aidha wamekuwa wakiwafokea wagonjwa na kuwadhalilisha kinyume na maadili ya kazi yao.

Kufuatia hali hiyo, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Seif Shekalaghe kufanya uchunguzi wa kina katika Hospitali hiyo ili kubaini chanzo cha changamoto hizi na hatimaye kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi kwa wale watakao bainika kuhusika ama kusababisha changamoto hizi.

Ikumbukwe kuwa, mapema Desemba 20, 2025 yaliibuka madai mtandaoni kutoka kwa baadhi ya watu yakibainisha kuwa wamekwenda kwenye Hospitali hiyo kupata huduma na kuambiwa watafute huduma sehemu nyingine kwani mashine za X-rays zilikuwa hazifanyi kazi.