Baada ya kupata ujauzito, swali la kwanza ambalo wanawake wengi huanza kuuliza ni lini hasa waanze kuhudhuria kliniki za ujauzito.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwanamke hushauriwa afike kliniki walau mara 4 kwenye kipindi cha ujauzito wake.
Mwanamke hushauriwa kufika kliniki haraka, pindi tu anapojihisi kuwa ni mjamzito. Hata hivyo, mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) husisitiza umuhimu wa kufika kliniki kwa mara ya kwanza kabla ya wiki ya 14 ya ujauzito.
Kwa hesabu ya miezi, hii ni sawa na miezi 3 ya mwanzo.
Mgawanyiko wa awamu za mahudhurio
Kwa kufuata kanuni na ushauri wa Shirika la Afya duniani (WHO), mahudhurio haya manne yanapaswa kuwa kwenye utaratibu ufuatao-
- Hudhurio la kwanza ndani ya miezi mitatu ya mwanzo (Kabla ya wiki 14)
- Hudhurio la pili kati ya wiki 24-28
- Hudhurio la tatu wiki ya 32
- Hudhurio la nne wiki ya 36
Kwa mwanamke anayetaka kuhudhuria zaidi ya hapo hakatazwi kufanya hivyo, anaweza kwenda kliniki mara nyingi kadri anavyoona inafaa.
Faida za Kliniki
Sio tu kuwa mwanamke anapaswa kuhudhuria kliniki, bali anapaswa kuanza mapema mahudhurio yake, walau kabla ya wiki ya 14 ya ujauzito.
Hudhurio la kwanza la kliniki hufaa afike na baba wa mtoto ili waweze kuchunguzwa na kushauriwa kwa pamoja juu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na uleaji wa ujauzito huo.
Mahudhurio ya kliniki husaidia kukinga, kugundua na kutibu changamoto mbalimbali zinazoweza kuwa hatari kwa afya ya mama na mtoto. Ni muhimu kwa kuwa husaidia kugundua mapema changamoto za uzazi, kupanga namna bora ya kujifungua, kupata chanjo zote muhimu, mfano tetenasi (Pepopunda) pamoja na kupima magonjwa ya zinaa yanayoweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto.
Pia, husaidia kujiandaa na hali yoyote ya dharura inayoweza kujitokeza wakati wa ujauzito, kuziba upungufu wa virutubisho na upungufu wa damu, kutoa usaidizi wa elimu ya uzazi, kijinsia na kisaikolojia kwa mama pamoja na lishe kwa mtoto pamoja na kupata dawa za kuzuia Malaria kali wakati wa ujauzito.
Tafiti zimeweka bayana kuwa uhudhuriaji wa kliniki huongeza ufahamu kwa mama katika kumtunza mtoto pindi azaliwapo, pia hupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa mama mjamzito.
Madhara ya Kutokudhuria Kliniki
Sio jambo zuri kutokuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito. Miongoni mwa madhara yake ni kupatwa na upungufu mkubwa wa damu, kuongeza nafasi ya kujifungua watoto njiti, wenye uzito mdogo au waliofariki pamoja na kutokupata nafasi ya kupanga mapema njia nzuri ya kujifungua pamoja na kushughulikia dharura zote za uzazi.
Aidha, huhatarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kutokupata nafasi ya kutosha ya kupima magonjwa ya zinaa na magonjwa mengine mfano presha, kisukari na kifafa cha mimba, kutokupata chanjo pamoja na virutubisho muhimu kwa ukuaji bora wa mtoto.
Kumbuka kuwa zama zimebadilika sana, sio vyema kutumia historia ya wazazi, ndugu wa karibu au marafiki kwenye kuamua mahudhurio ya kliniki yako. Kuwa wewe mwenyewe.
Muhtasari
Ukosefu wa elimu ya kutosha ni sababu inayotajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake katika kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito.
Kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hili, baba wa mtoto anapaswa kuambatana kila mara na mama mjamzito ili waweze kupatiwa elimu ya mtoto kwa pamoja.
Husaidia pia kugundua changamoto zinazoweza kuhatarisha afya ya mtoto hasa kama watakuwa na makundi tofauti ya damu, hivyo kuepusha madhara ya kudumu ya kupoteza ujauzito mwingine kila watakapotaka kupata mtoto.

